Kuharibika kwa mimba ni hali ya
mwanamke kupata ujauzito na ukatoka kabla ya muda wake ambapo tatizo hili
huangaliwa kabla ya kutimiza wiki 20 tangu kutungwa kwake.Hali hiyo inapotokea
huitwa kuwa mimba imetoka au imeharibika (Miscarriage).
Hali hii ya mimba kuharibika
inakuwa tofauti kabisa na utoaji mimba ambapo kitendo cha kutoa mimba
kinafanywa na binadamu kwa makusudi na huwa amedhamiria kufanya hivyo.
Tatizo la mimba kuharibika ni
kwamba mtoto anakuwa hawezi kujitegemea mwenyewe kwa mahitaji
yanayotakiwa ikiwa ni pamoja na kupumua, hivyo hali hiyo ya kutojitegemea
husababisha kifo cha motto huyo.
Sababu za mimba kutoka
Miongoni mwa sababu zinazosababisha
mimba kutoka ni pamoja na umri mkubwa ambapo kwa kawaida mwanamke anapofikisha
umri wa miaka 35 au zaidi misuli(sphencters) ya mji wa uzazi hulegea na
kupunguza nguvu za kuweza kuhimili na kutunza kiumbe kinachokuwa ndani ya mji
wa uzazi, hivyo kusababisha mimba kutoka.
Hitilafu katika kizazi ambayo
huwa katika mfuko wa mimba(uterus) ambao muundo wake siyo wa kawaida.Wanawake
wenye tatizo kama hili huwa na hatari kubwa ya mimba kuharibika kabla ya miezi
tisa.
Aidha maambukizi ya fangasi au
bakteria husababisha misuli ya kizazi kushambuliwa hivyo kupoteza uwezo wake wa
kuhifadhi ujauzito hivyo mimba kuharibika.
Miongoni mwa sababu zingine zinazosababisha
mimba kuharibika ni matatizo ya vinasaba(genetic factors). Hali hiyo hutokana
na hitilafu katika kromosomu(cromosomal abnormalities) ambayo husababisha
vinasaba kuwa katika hali isiyo ya kawaida ambayo hali hiyo ni miongoni mwa
sababu kubwa zinazosababisha mimba kutoka kabla ya kutimiza wiki 13.
Hii husababisha damu ya mama kushindwa
kuendana na damu ya mtoto hivyo kutokea kwa madhara ambayo humdhuru mtoto na
kumfanya ashindwe kuhimili hali ya tumboni kwa mama hivyo kutoka nje.
Pia ukosefu wa homoni ya
progesterone ambayo hufanya kazi kubwa tangu kutungwa kwa mimba hadi mtoto
kuzaliwa ambayo huchochea uimara wa ukuta wa placenta ambao mtoto
hujishikiza.
Upungufu wa homoni hii
husababisha ukuta wa mji wa mimba kushindwa kuhimili uzito wa mtoto, hali
ambayo husababisha ujauzito kuharibika kabla ya muda wake.
Sababu nyingine ni utumiaji wa
pombe kali, sigara na dawa za kulevya. Utumiaji wa vitu hivi huchangia mimba
kutoka kutokana na kemikali nyingi zilizomo. Hivyo mwanamke mjamzito hushauriwa
kutotumia vitu vyenye kemikali, ili kulinda afya yake na mtoto aliyeko
tumboni.
Pia baadhi ya vyakula na
vipodozi huwa vina kemikali ambazo hupelekea shingo ya kizazi kulegea na kadiri
mimba inavyozidi kukua huendelea kuachia na kusababisha mimba kushuka,hali
inayosababisha mimba kuharibika.
Dalili za mimba kuharibika(symptoms of a miscarriage)
Dalili zinazojitokeza
wakati wa mimba kuharibika ni pamoja na kutokwa na damu sehemu za siri. Hiyo ni
dalili kubwa ya mimba kuharibika ambapo damu hiyo hutoka sawa na mwanamke
anayekuwa kwenye siku zake.
Maumivu katika viungo ambayo
huwa makali katika kiuno, nyonga na tumbo chini ya kitovu ambapo maumivu hayo
huanza taratibu, lakini huongezeka kadiri muda unavyozidi kusonga mbele ambapo
hali hiyo huambatana na kutokwa damu sehemu za siri.
Dalili nyingine ni kutokwa na
uchafu sehemu za siri. Hii ni dalili kubwa ya mimba kutoka. Mama mjamzito
kuanza kutokwa na uchafu mwingi wenye rangi sambamba na mabonge ya damu.
Kupata maumivu ya kiuno huku
ukisikia maumivu hayo yanashuka chini kwa nguvu fahamu fika mimba yako inaweza
kutoka muda wowote.
Madhara yatokanayo na kuharibika kwa mimba
Iwapo mama mjamzito amepata
tatizo hili na hajapata tiba sahihi kama kuna mabaki tumboni yanaweza
kusababisha madhara mengine ikiwemo kizazi kuoza au kusababisha matatizo
mengine kwenye mji wa mimba.
Miongoni mwa madhara yanayoweza
kumpata mama ambaye mimba imeharibika ni pamoja na kizazi kuharibika ikiwa mama
hatasafishwa vizuri tumboni baada ya mimba kuharibika.
Madhara mengine ni kuugua
mfululizo baada ya ujauzito kuharibika pamoja na kushambuliwa na madhara
mfululizo baada ya ujauzito kuharibika.
Pia mama anaweza kupata madhara
ya kisaikolojia ambayo yanachukua muda mrefu kusahaulika hasa pale wanapokutana
na wanawake wajawazito au wenye watoto.
Matibabu
Mwanamke mwenye tatizo la
kuharibika kwa mimba anaweza kupata matibabu kwa njia mbalimbali
kutegemea na mgonjwa husika.
Matibabu hayo hupatikana
hospitalini ambapo mwanamke anatakiwa kuwahi pale anapoona dalili hatarishi.
Kwa yule mwenye historia ya
kuharibika kwa mimba na tayari ana mimba atapata matibabu tofauti na yule
mwenye tatizo hilo, lakini hana mimba kwa muda huo.
Ushauri
Dalili zilizotajwa hapo juu
peke yake hazitoshi kuonyesha kuwa mimba imeharibika bali mama mjamzito
anapoona dalili moja kati ya hizi au zote hata hali ambayo haielewi anatakiwa
kuwahi hospitalini ili kuweza kupata vipimo.
Endapo mama huyo atachelewa
atakuwa anajiweka katika hali mbaya kutokana na sumu inayotokana na kiumbe
kilichoharibika na kusababisha matatizo kwenye mfuko wa uzazi ikiwemo
ugumba.
Mwanamke yeyote ambaye hajapata
tatizo hilo anashauriwa kula vyakula kama maboga, mboga za majani na
vyakula vyote vinavyojenga mwili.Pia wanatakiwa kuacha matumizi ya vipodozi
vyenye kemikali pamoja na uvutaji wa sigara na dawa za kulevya ili
kujikinga na tatizo la kuharibika kwa mimba.
No comments:
Post a Comment