Monday, 27 July 2015

Faida na Aina ya Mazoezi kwa Wanawake Wenye Ujauzito


Wanawake wenye ujauzito hushauriwa kitaalamu kufanya mazoezi kwani yana faida nyingi kwa wanawake hao. Kwanza, mazoezi huongeza hisia za mwili wa mama, humsaidia mama kupata usingizi na hupunguza maumivu ya mgongo. Aidha, mazoezi kwa mama mjamzito humwandaa mama na kumpa nguvu wakati wa kujifungua.
 Mjamzito anapofanya mazoezi, hutanua misuli ya kiuno na ile ya njia ya uzazi. Mazoezi  huipa  nguvu na uvumilivu  misuli wakati wa kujifungua. Misuli inapokuwa mwepesi, huwa ni rahisi mwili huo kurudi katika umbile lake la awali mapema mara baada ya kujifungua.
Mjamzito anapofanya mazoezi, huufanya moyo wake kupata mapigo mazuri na kuchochea mzunguko mzuri wa damu. Aidha mazoezi humfanya pia mama mjamzito asiongezeke uzito na kumuepusha na shinikizo la damu. Mazoezi haya huepusha wingi wa mafuta mwilini (lehemu),  hivyo kuzuia maradhi ya mishipa ya damu kwa mjamzito. Mzunguko mzuri wa damu huepusha damu kuganda  tendo linalosababisha  kukwama kwa  usambazaji wa damu mwilini, (moyo, ubongo na mapafu).
Mazoezi yafuatayo ni mazuri kwa mama anayetarajia kupata mtoto. Ingawa baadhi ya mazoezi yanaweza yasiwe na matokeo mazuri kwa mama ambaye amebakiza siku chache za kujifungua.
Hata hivyo, mama anatakiwa kuhakikisha anawasiliana na daktari wake kabla hajafanya uamuzi wa aina ya mazoezi ya kufanya.

Kutembea:
Haya  ni miongoni mwa mazoezi mazuri kwa ajili ya kupunguza maradhi ya moyo. Kutembea kunamsaidia mjamzito asitetemeke magoti na kifundo cha mguu.
 Kutembea kunaweza kufanyika popote, hakuhitaji zana, wala fedha. Labda viatu visivyo na kisigiono. Kutembea kunaweza kufanyika hata katika hatua za mwisho za ujauzito.
 Kuogelea:
Wataalamu wa afya wanashauri kuwa kuogelea ni zoezi zuri  na salama pengine kuliko yote kwa wajawazito. Kufanya hivyo  kunaipa mazoezi misuli mikubwa ya mwili hasa ya mikono na miguu.
 Pia, kuogelea kunaepusha maradhi ya moyo na humfanya mjamzito kujihisi mwepesi licha ya kilo za ziada alizonazo.
Kucheza muziki:
Unaweza kuyafanya mapigo ya moyo wako kuwa katika hali nzuri kwa kucheza muziki. Waweza kutumia chumba chako cha kulala au sebule kucheza muziki wowote uupendao.
Aidha waweza kutembelea madarasa ya muziki au mazoezi kwa njia ya muziki.
Mambo ya kuzingatia kabla ya kufanya mazoezi
1. Wasiliana na daktari wako ili akupe ushauri
2. Epuka mazoezi yanayoweza kukupotezea ukinzani,au kukufanya udondoke.
3. Vaa mavazi mapana, ambayo hayatakufanya ukose nafasi ya kufanya mazoezi. Epuka nguo zinazobana.
4. Kula vizuri. Kwa kawaida mama mjamzito huongezeka uzito kadri mtoto anavyokua. Anapofanya mazoezi mwili wake huhitaji kalori za ziada kwa ajili ya watu wawili.
5. Kunywa maji ya kutosha. Mama mjamzito anayefanya mazoezi anatakiwa kunywa maji, kabla, wakati na baada ya mazoezi. Mjamzito asipofanya hivyo anaweza kuongeza joto la mwili na kusababisha madhara kwa mtoto aliye tumboni.

No comments:

Post a Comment