Tuesday 18 August 2015

Tatizo la Mwanamke Kutokwa Uchafu Ukeni (Vaginitis) na Jinsi ya Kulitibu

Picture of Human Vagina
Kitaalamu hali ya mwanamke kutokwa na majimaji (vaginal fluids) yenye rangi nyeupe au ya njano, ni hali ya kawaida na wala siyo tatizo endapo majimaji hayo siyo mazito sana na wala hayatoi harufu mbaya. Lakini endapo majimaji yanayotoka yapo katika hali ya ute mzito wenye rangi nyeupe au kahawia, yanatoa harufu kali na yanawasha, basi hiyo ni ishara ya ugonjwa uitwao Vaginitis.
Majimaji au ute unaoteleza kutoka sehemu za siri ni njia inayowezesha viungo vya uzazi vya mwanamke kujisafisha na kuutoa uchafu wa seli zilizokufa na mabaki ya damu ya hedhi nje ya mwili. Pia huvikinga viungo vya uzazi dhidi ya maambukizi ya bacteria au fangasi wanaosababisha magonjwa. Kwa kawaida huwa hayatoi harufu na huwa na rangi nyeupe au ya njano. Pia huwa na asidi ya Lactic ambayo huzuia kuzaliana kwa vijidudu vya maradhi na huzalishwa kwenye tezi za Bartholin (Bartholin's glands) zilizopo kwenye shingo ya mlango wa uzazi (Cervix).
Kwa kawaida, mwanamke hutoa kiasi cha gramu 2 za seli zilizokufa kutoka kwenye mji a uzazi na gramu 3 za ute mwepesi kila siku. Kiwango hiki huweza kuongezeka au kupungua kutegemeana na mzunguko wa hedhi. Kuna wakati ute huwa mwepesi na unaovutika (kama ute wa yai la kuku) na kuna wakati huwa mzito kiasi na wenye rangi ya njano. Ute huu ni wa kawaida na huwatoka wanawake wote hususan baada ya kuvunja ungo.
CHANZO/SABABU
Kuna sababu nyingi ambazo husababisha mwanamke kutoa ute au majimaji yasiyo ya kawaida kutoka kwenye sehemu zake za siri. Maambukizi ya bacteria wanaosababisha magonjwa kama Trichomoniasis, Candidiasis, Gonorhear au uambukizo wa bacteria Candida albicans, Vaginosis Bacteria n.k husababisha mwanamke kutokwa na uchafu unaoambatana na harufu mbaya.
Pia mabaki ya vitambaa, tissue au pedi ambazo hazikutolewa wakati wa hedhi huweza kusababisha tatizo hili. Usafi wa sehemu za siri usipozingatiwa hususani mwanamke anapokuwa kwenye siku zake za hedhi, huweza kuwa mazalia mazuri ya bacteria wanaosababisha harufu mbaya.
DALILI
Wanawake wenye tatizo la Vaginitis huwa na dalili kubwa ya kutokwa na
uchafu usiyo wa kawaida  kutoka sehemu za siri. Uchafu huu huwa unatoa harufu kali kama shombo ya samaki au kitu kilichooza na huambatana na maumivu makali ya tumbo chini ya kitovu. 
Wakati mwingine uchafu wenye rangi kama ya kijani hutoka,kuwashwa sana sehemu za siri, mgonjwa asipopatiwa tiba haraka husababisha vidonda sehemu za siri kwa sababu ya kujikuna kutokana na mwasho anaoupata.
 Kuna wakati mwingine  mwanamke anatokwa na ute uliochanganyikana na damu hata kama hayupo kwenye siku zake, hii ni dalili nyingine ya Vaginitis. Mgonjwa pia anaweza kusikia maumivu makali wakati wa tendo la ndoa, hali ambayo pia inaweza kusababishwa na kuingiwa kwa bakteria katika mji wa uzazi.
Bakteria hao huweza kusababisha siyo harufu tu, bali mgonjwa anaweza kutokwa na usaha sehemu hiyo ya siri.
MATIBABU
Tatizo hili hutibika hospitalini baada ya vipimo vya kitaalamu kuchukuliwa na mtaalamu mwenye uzoefu wa kutosha juu ya magonjwa ya wanawake. Daktari anaweza kumpa mgonjwa dawa za kupaka na dawa za kumeza ambazo huweza kumaliza tatizo hili.
Pia unaweza kutumia njia za asili kutibu tatizo la viginitis. Njia hizo ni pamoja na hizi zifuatazo:
1.    Kitunguu swaumu (Garlic): Menya punje kadhaa za kitunguu swaumu na zifunge kwenye kitambaa laini ambacho nyuzi zake hazikubanana sana. Kisha mwanamke mwenye tatizo la viginitis akiingize ukeni na alale nacho usiku kwa siku sita (six nights) hivi. Kitunguu swaumu kina compound iitwayo allicin ambayo ina uwezo wa kuua fangasi waitwao Candida albicans ambao husababisha maambukizi ya vaginal yeast (Candida).
2.    Teatree oil au Cardamom oil (mafuta ya iliki): Teatree na Iliki vina kemikali iitwayo terpinen-4-ol ambayo hutumiwa kutengeneza dawa kutibu candida (yeast infections). Dawa hizo ni pamoja na nystatin (Mycostatin) na clotrimazole (Gyne-Lotrimin). Iliki ina kiwango cha terpinen-4-ol mara mbili zaidi ya teatree. Changanya matone mawili au matatu ya teatree oil au mafuta ya iliki na yogurt kijiko kimoja kikubwa (tablespoon). Chovya kitambaa laini au pamba kwenye mchanganyiko huo na kitambaa hicho kiweke ndani ya uke kila siku wakati wa kulala kwa muda wa siku sita.
3.    Siki ya Apple (Apple cider vinegar): hii utaipata madukani au supermarkets. Weka siki hiyo vikombe vitatu kwenye maji vuguvugu yaliyo kwenye sinki la kuogea. Kisha kaa humo ndani ya sinki kwa muda wa dakika 20 hivi huku ukiwa umepanua mapaja yako kuruhusu maji kuingia ndani ya uke. Siki hiyo husaidia kurejesha hali ya asidi (normal vaginal acidity) ambayo husaidia kuondoa tatizo la candida, trichomonas na gardnerella.

USHAURI
Mara nyingi watalaamu wanashauri kuwa ni makosa kutumia dawa hususan zile za viwandani bila kupata ushauri wa kitaalamu kutoka kwa daktari aliye na ujuzi wa magonjwa hayo na siyo kupewa dawa na wauzaji wa maduka ya dawa.
Watu wengi wana kawaida kwenda kwenye duka la dawa na kupewa dawa na muuzaji bila kupimwa. Kumbuka unaweza kupewa dawa ambayo siyo ya ugonjwa wako. 
Nawashauri pia wale wanawake wenye kawaida ya kutumia pafyumu au kuweka dawa sehemu za siri kwa lengo la kuzifanya kuwa ndogo, waache kufanya hivyo kwani madhara yake ni makubwa sana kiafya likiwemo hilo la kutoa harufu mbaya sehemu hizo na zinaweza kusababisha madhara makubwa katika njia ya uzazi. Aidha inashauriwa kuepuka matumizi ya sabuni zenye kemikali zinazotumika kuoshea ukeni au kutumia lubricants zenye kemikali wakati wa kufanya mapenzi kwani kemikali hizo huondoa hali ya asili ya uke na pia huua bacteria rafiki ambao hupambana na vimelea vya magonjwa sehemu za uke.

1 comment:

  1. DAWA ZA UTI ..UGUMBA..UCHAFU UKENI..HEDHI ISIYO NA MPANGILIO..NGUVU ZA KIUME..KUREFUSHA NA KUNENEPESHA UUME..NA MARADHI MENGINE MBALIMBALI ONANA NA DR KUPITIA NO 0764839091...TANGA

    ReplyDelete