Wednesday, 26 August 2015

Mwanamke Kabiliana na Tatizo la Kuota Ndevu kwa Kufanya Haya

Wasichana wanapoota ndevu nyingi hukabiliwa na changamoto za kisaikolojia na ulimbwende. Mitazamo na mila nyingi za kijamii katika bara la Afrika, bado zinakumbatia unyanyapaa wa wazi au wa kificho kwa wasichana wanaoota ndevu nyingi. Msichana mwenye ndevu nyingi anavuta hisia na macho ya wanaume na wanawake wenzake pia kiasi kwamba anatazamwa kwa namna ambayo wakati mwingine inamnyima raha. Wakati mwingine wanaume hawapendi kuoa wasichana wenye ndevu nyingi kutokana na mwonekano unawafanya wasichana hao kuwa kama wanaume.

Katika hali ya kawaida msichana anatazamiwa asiwe na nywele nyingi kwenye kidevu, juu ya mdomo wake, kifuani, tumboni na mgongoni. Na hata akiwa nazo basi ziwe malaika zisizokuwa na rangi nyeusi iliyokolea na kuwa ngumu kama za wanaume.

Mwanamke anapokuwa na nywele nyingi sehemu hizo humaanisha kuwepo kwa hitilafu za kijenetiki au dosari za ulinganifu wa vichocheo vya jinsia mwilini mwake. Wasichana wengine maumbile yao yanayotokana na vinasaba yanawafanya wawe na nywele nyingi mwilini, hali hii kitabibu hujulikana kama ‘hypertrichosis’.Dosari za ulinganifu wa vichocheo vya kijinsia kwa wasichana zinaweza kusababishwa na:-
(1) Kuzalishwa kwa wingi kwa vichocheo vya ujinsia toka katika mifuko ya mayai.
(2) Uvimbe katika mifuko ya mayai (ovarian tumors)
(3) Matumizi ya dawa za uzazi wa mpango zenye vichocheo pia zinaweza kuwa chanzo cha tatizo hili kwa baadhi ya wasichana. Dawa hizi husababisha ongezeko la vichocheo bandia vya ujinsia kuwa vingi katika mwili wa msichana.
(4) Matumizi ya dawa na vipodozi vyenye viambato vya dawa kama testosterone na steroid zingine pia husababisha tatizo hili endapo dawa hizi zitatumiwa kwa muda mrefu.
(5) Uvimbe wa tezi ya Adrenali iliyo juu ya figo pia unaweza kusababisha tatizo hili.
(6) Unene wa kupindukia (obesity) kwa wasichana pia unaweza kusababisha ongezeko la kichocheo cha kiume (Androgen) mwilini mwa msichana kutokana na nyama zenye mafuta mengi kugeuza kichocheo cha kike cha estrogen kuwa kichocheo cha kiume cha androgen. Androgen inapokuwa nyingi mwilini husababisha msichana kuwa na tabia za kiume ikiwa ni pamoja na kuota ndevu na kuwa na sauti nzito.
(7) Matumizi makubwa na holela ya baadhi ya dawa zenye kemikali kama vile Danazol, Cyclosporin na zingine pia husababisha tatizo hili.Ni vizuri kwa wasichana kuepuka matumizi ya dawa bila kupata ushauri wa kitabibu.
(8) Ikumbukwe kuwa wakati mwingine kunakuwepo na hali ya ulinganifu wa vichocheo vya ujinsia mwilini kama kawaida, lakini tatizo likawa ni mwitikio wa hali ya juu wa nywele (oversensitivity) kwa kiasi cha kawaida cha kichocheo cha kiume kilichoko mwilini mwa msichana (androgen).Katika hali hii, msichana pia anaweza kuwa na nywele nyingi mwilini kuliko kawaida.

Dalili zinazo ambatana na kuota ndevu kwa msichana
• Kuota chunusi nyingi.
• Kutokupata damu ya hedhi kama kawaida. Wakati mwingine msichana hupata damu pungufu sana, kutoiona kabisa au kupata hedhi yake bila mpangilio maalumu.
• Matatizo mengine yanayosababisha ndevu kuota kwa wingi pia yanaweza kusababisha ugumba (kushindwa kupata ujauzito na kuzaa watoto).
• Kusinyaa kwa matiti na mfuko wa mji wa mimba.
• Kututumuka na kunenepa kwa kinembe kuliko kawaida (enlargement of the clitoris).
• Kuwa na sauti nzito na wakati mwingine kisanduku cha sauti (Adam’s apple) hunenepa kama cha wanaume.
• Mtawanyiko wa nywele mwilini huwa kama wa kiume, pamoja na ndevu msichana huota nywele kifuani, tumboni, mapajani, mgongoni, miguuni na mikononi kwa wingi. Wengine pia huota nywele nyingi kwenye makalio na kuzunguka sehemu ya njia ya haja kubwa na hali hii ya msichana kuwa na nywele nyingi mwilini, hujulikana kama “hirsutism”.

Jinsi msichana anavyoweza kukabiliana na tatizo la ndevu
• Kwanza kabisa msichana anatakiwa kuelewa kuwa kuota ndevu sio dhambi na wala si kosa, hivyo basi ndevu zisiwe chanzo cha msongo wa mawazo.
• Msichana asiache ndevu zikawa ndefu kama za wanaume kwani zinavuta hisia za watu kumwangalia angalia kiasi kwamba zinaweza kusababisha matatizo ya kisaikolojia. Ndevu zikatwe na kuwa fupi kadri inavyowezekana kwa wakati wote. Mkasi au cream ya kuondoa nywele inaweza kutumika kwa lengo hili. Ile dhana ya wanawake wengi kwamba ndevu zikinyolewa zinaongezeka maradufu haina ukweli wowote wa kisayansi.
• Ni bora wasichana wakajiepusha na matumizi ya vipodozi vyenye viambato vyenye dawa za magonjwa ya ngozi.
• Ndevu zising’olewe kwa vidole, hii inaweza kusababisha uambukizo wa bakteria katika ngozi kwa urahisi na kuleta matatizo ya kiafya.
• Wasichana waepuke matumizi ya dawa zenye steroid bila kupata ushauri wa kitaalamu toka kwa wahudumu wa afya na maswala ya tiba.
• Kufanya mazoezi ya mwili na kudhibiti unene wa mwili pia husaidia katika udhibiti wa tatizo hili.
• Endapo nywele zimetapakaa kwa wingi miguuni na mikononi na kuleta muonekano wa kiume ni bora kuvaa nguo ndefu zinazofunika mwili vizuri ili kuepuka msongo wa kisaikolojia ambao unaweza kutokea kutokana na mtazamo hasi wa kijamii.
• Wakati wote jivunie kuwa msichana, usikubali kitu chochote kikuondolee hisia zako za kuwa msichana kamili. Afya ya mwili na roho huanza na afya ya akili. Jitambue, jipende, jiheshimu na jiamini kwani wewe ni msichana kama walivyo wasichana wengine.


No comments:

Post a Comment