Relaxer
ni dawa ya nywele inayofanya nywele za mtu mwenye ngozi nyeusi wa asili ya
Afrika zilainike na kunyooka kama nywele za wazungu, waasia au waarabu. Watu
wengi hasa wanawake wanapenda kutumia relaxer ili nywele zao ziwe na mwonekano
tofauti. Kihistoria matumizi ya relaxer yalianza kama matokeo ya watu weusi
kubaguliwa. Watu weusi walipoona hivyo waliamua kuiga maisha ya kizungu ili
kufanana fanana na wazungu kwa rangi ya ngozi na nywele ili wathaminiwe na
kupewa upendeleo wa kupata fursa za mafanikio na watawala wetu enzi za ukoloni.
Wakoloni waliwapendelea watu walioipokea kasumba hii kwa mikono miwili.
Siyo
lengo langu kuingia kwa undani katika historia, ila ninajaribu kukupa picha ya
chimbuko la matumizi ya kitumwa ya dawa zinazodhuru afya ya watu weusi kwa
kiwango kikubwa. Pia kupitia mada hii najaribu kukupa uelewa ili unapofanya
uchaguzi wa kutumia au kuacha, uchaguzi wako ujengwe katika uelewa sahihi na
siyo katika mkumbo au msukumo wa kijamii unaowaona watu wasiotumia dawa hizi
kama washamba.
Sayansi
inaonyesha kuwa matumizi ya relaxer za nywele yanaweza kusababisha au kuongeza
hatari ya kupata magonjwa ya moyo, kupungua kwa uwezo wa kiakili katika
kufikiri na kupambanua mambo, kuungua kwa ngozi ya kichwa na muwasho wa ngozi.
Matatizo mengine ni saratani ya matiti, mabonge katika mji wa mimba
(Leiomyomata), upungufu wa kinga ya mwili na kubalehe mapema kwa wasichana.
Katika utafiti uliofanywa na wanasayansi Lauren A. Wise na wenzake (Wise et al,
2012: Hair Relaxer Use and Risk of Uterine Leiomyomata in African-American
Women) na kuchapishwa katika jarida la American Journal of Epidemiology (2012)
vol. 175(5):432-440, ilibainika kuwa matumizi ya relaxer yanaongeza hatari ya
kupata mabonge katika mfuko wa kizazi.
Mabonge
yanaweza kusababisha ugumba hasa pale yanapokuwa makubwa na kulazimisha tiba ya
upasuaji ya kuondoa kizazi (hysterectomy). Katika jamii za wanawake wanaotumia
relaxer kwa kiwango kikubwa, chanzo kikubwa cha upasuaji wa kuondoa mfuko wa
uzazi ni mabonge. Inasemekana kuwa katika nchi ya Marekani wanawake weusi
wanakabiliwa na tatizo la mabonge mara mbili hadi mara tatu zaidi ya wanawake
wengine. Hii inaweza kuwa na uhusiano wa moja kwa moja na matumizi makubwa ya
vipodozi kama relaxer.
Viambato
vilivyomo ndani ya dawa hii hupenya na kuingia katika mfumo wa damu na kwenda
kuvuruga mfumo wa vichocheo vya ujinsia hasa homoni za kike. Relaxer nyingi za
nywele zina kiwango kikubwa cha kemikali kama vile lye (Sodium hydroxide au
Caustic soda), calcium hydroxide, guanidine carbonate, thioglycolic acid salts
na monobutyl phthalate.
UCHAGUZI NI WAKO, KUENDELEA KUTUMIA RELAXER AU
KUACHA!
No comments:
Post a Comment