Friday 7 August 2015

Mazoezi ya Kuondoa Kitambi


Image result for sit ups exercise photos

Kutokana na kufumka kwa maradhi mbalimbali baadhi ya watu wamekuwa wakihangaika kutafuta njia rahisi za kupunguza ama kuondoa vitambi hivyo na uzito uliopitiliza. Wapo waliamua kukaa na njaa na wengine kutumia dawa kali wakilenga kufikia malengo yao ambayo ni kupunguza uzito.
Lakini kuwa na kitambi ama ongezeko la uzito linaweza kuondolewa kwa njia rahisi sana tofauti na unavyodhani. Tena njia isiyohusisha hata chembe ya dawa itakayoweza kukuletea madhara baadaye. Licha ya wataalamu wengi kusisitiza kuwa kitambi au ongezeko la uzito ni matokeo ya ulaji mbovu, lakini ukweli utabaki kuwa mazoezi kwa sehemu kubwa yana nafasi kubwa ya kupunguza uzito na kuondoa kitambi.

Profesa Christine Rosenbloom, mtaalamu wa lishe kutoka Chuo Kikuu cha Georgia, Marekani anasema kupunguza mafuta mwilini kunaendana na ulaji wa chakula bora pamoja na mazoezi ya kila siku.
“Unatakiwa kufanya mazoezi kwa muda usiopungua dakika 60. Kwa kufanya hivi utaweza kuondokana na matatizo ya unene ama mafuta tumbo,” anasisitiza.
Naye Profesa Michael Jensen wa Kliniki ya Mayo anasema, mazoezi ya viungo yana nafasi kubwa sana ya kuutengeneza mwili wako katika hali nzuri zaidi na pia kuufanya uwe mwepesi pia.
Ni muhimu kuelewa kuwa unapoushughulisha mwili wako, unauweka katika nafasi ya kuunguza mafuta na hivyo kujiweka kwenye nafasi ya kuondokana na unene. Ikiwa utafanya mfululizo ni wazi mwili hautakuwa na mlundikano wa mafuta.
Umuhimu wa mazoezi
Wataalamu wanasema watu wengi huamini kuwa unene ni matokeo ya kula vyakula vyenye kalori nyingi. Hivyo kwa kupunguza kalori wanaamini kuwa itakuwa ni njia rahisi ya kupunguza uzito wa mwili.
Licha ya kuamini hivyo lakini wataalamu wanasisitiza kufanywa kwa mazoezi kwani ndiyo njia pekee itakayoufanya mwili wako kukubaliana na mpango mzima wa kupunguza hizo kalori huku ukiipa nafasi misuli yako kuurudisha mwili katika hali inayotakiwa.
Wanasema kupunguza kalori kwa njia isiyokuwa na mazoezi huwaweka wahusika katika hali ya kunenepa zaidi endapo ataamua kurudi katika ulaji wake wa kawaida.
Kujenga misuli
Jambo la muhimu unalopaswa kufahamu unapoamua kuanza mpango wa kupunguza uzito na mafuta mwilini ni kujua ni nini hasa unatakiwa kufanya. Kuwa na malengo ndiyo jambo la msingi litakalokusaidia kukutia nguvu na hata kufanikiwa.
Watafiti kutoka maabara ya Chuo Kikuu cha San Diego Marekani, waliunganisha mazoezi mbalimbali ya tumbo. Matokeo yake waligundua kuwa mazoezi ya tumbo yana nafasi kubwa sana ya kuikaza misuli inayozunguka tumbo na hivyo kurahisisha zoezi la kupunguza kitambi na kulifanya tumbo kuwa bapa.
Yafuatayo ni mazoezi matano muhimu katika kupunguza mafuta tumboni:
Zoezi la baiskeli
 Hili husaidia kukata tumbo sehemu ya chini na ya juu. Unachotakiwa kufanya ni kulala chali. Kisha chukua mikono shika kichwani kwa nyuma upande wa kisogoni. Wakati umelala kunja miguu yako na kisha jinyanyue hadi kujikunja mfano wa ‘c’ iliyolalia mgongo. Fanya hivyo mara 12 hadi 16.
Zoezi la “Sit ups’
Ukiwa umelala chini. Nyoosha miguu yako. Kisha nyoosha juu mikono yako. Jinyanyue na kugusa miguu yako. Fanya hivyo mara 20 hadi 30
Zoezi la kunyoosha tumbo
Kaa chini na nyoosha miguu yako huku ukiitanua hadi kufikia uwezo wako wa mwisho. Geuza kifua chako hadi uweze kuona upande wa nyuma yako kwa uzuri zaidi bila kugeuka mwili mzima. Fanya hivyo huku ukibadilisha upande. Hakikisha unafanya mara 10 kwa kila upande, mkono wako wa kulia uweze kuzunguka.
Zoezi kunyonga miguu
Hili ni maalumu kwa ajili ya tumbo la chini. Lala chali na kisha nyanyua miguu yako. Anza kuinyonga kama unavyofanya unapoendesha baiskeli. Fanya hivyo mara 20. Utasikia maumivu katika tumbo lako la chini
Zoezi la kuzungusha kiuno
Simama na kisha shika mikono yako kiunoni. Tanua miguu yako ili kusimama imara. Zungusha mwili wako kuanzia kwenye kiuno kuja juu.

1 comment: