Thursday, 23 July 2015

Siri ya urembo halisi wa mwanamke

UREMBO HALISI WA MWANAMKE UNAANZIA NDANI YAKO

Urembo unajumuisha mambo mengi kwa mwanamke tofauti na dhana za watu wengi wanaofikiri kwamba urembo ni kuvaa vizuri, kuonekana vizuri na hata manukato mazuri, kuwa na umbo zuri, na jinsi unavyoonekana kutokana na umbo lako. La hasha hivi ni vidokezo vya urembo kwa mwanamke.



Urembo halisi ni amani na utulivu uliopo ndani yako, hali hii ina faida katika moyo wako na mwili wako pia. Jambo la msingi hapa ni kuwa na amani kwa kuepukana na msongo wa mawazo na kuwa mwenye furaha muda wote. Hali ya msongo wa mawazo (stress) huleta maradhi mbalimbali kama vidonda vya tumbo (gastric ulcers), shinikizo la damu (blood pressure) na mengine mengi.


Katika maisha ya mwanamke yeyote mwenye kupenda urembo na muonekano mzuri  ni pamoja na kuepukana na magonjwa yanayoepukika kwa njia ya kua na amani na furaha muda wote kwa kujenga sura nzuri, umbo zuri lenye kupendeza pale unapovaa nguo ya aina yoyote au kupaka vipodozi vya aina yoyote ile.

Ni vyema tujiulize, je ni kiasi gani cha fedha tunatumia kila mwaka kununua nguo mpya, viatu vya gharama, vipodozi na mikoba? Bila shaka ni gharama kubwa lakini je, kuna gharama gani tunatumia kujenga furaha na amani ndani yetu? Jibu ni rahisi tu furaha na amani ni wewe mwenyewe pasipo gharama yoyote ile. Maswali haya yatakufanya wewe kama mwanamke mpenda urembo kupata njia thabiti za kuongeza urembo.

VIFUATAVYO NI VIDOKEZO VINAVYOONGEZA UREMBO WAKO KAMA MWANAMKE 

1. Kupata muda wa kutosha wa kupumzika ni muhimu kwa urembo wako, ni kweli kwamba sisi kama wanawake tunatumia muda mwingi kutimiza majukumu ya kifamilia kama mama, dada, watoto wa kike na hata wanawake ambao tuna majukumu ya kutimiza malengo fulani ya kimaendeleo mbali na familia yatupasa kupata muda wa kupumzika na kupata hewa safi kila baada ya shughuli mbalimbali za kila siku ili kujenga afya ya ngozi yako kimuonekano na akili pia.


2. Mazoezi ni nguzo muhimu katika urembo, kwa kufanya mazoezi kutakupunguzia uchovu na uzembe wa mwili, na hivyo kuuandaa mwili kupambana na magonjwa mbalimbali kama mafua na maumivu ya mwili. Mazoezi pia yanajenga umbo zuri kwa mwanamke kwa kupunguza mafuta mwilini na hivyo kuleta muonekano mzuri hata unapovaa nguo yako na kuvutia.

3. Maji ni muhimu katika kuongeza urembo wa ngozi yako kwani maji yanasaidia kuboresha tishu za ngozi na kufanya ngozi isiwe kavu kwa kuongeza unyevu katika ngozi. Pia maji yanasaidia kupunguza uzito mwilini na pia inashauriwa kwa mtu mwenye mafuta mwilini kujizoesha kunywa maji yenye vuguvugu ili kupunguza mafuta.

4. Jiwekee muda maalum kwa siku wa kutafakari uzuri wako. Jaribu kufumba macho hata kwa dakika tano kila siku na vuta taswira ya vitu upendavyo, waza umealikwa katika tamasha fulani na umevaa vizuri umependeza. Waza umejumuika na marafiki pamoja na ndugu, jamaa au marafiki, hii itajenga hali fulani ndani yako na kuongeza furaha na hivyo kuonekana mrembo zaidi machoni mwa watu kwa kuonyesha uso wa bashasha.
5. Tabasamu kila mara na jifunze kusaidia wengine wenye matatizo kwa kuwapa tabasamu, hii itajenga urafiki na watu tofauti na hivyo kupelekea amani na furaha kati yenu. Itakupa ujasiri kama mwanamke na kuwa kioo cha jamii kwa kusaidia wenye matatizo. Na kama kioo cha jamii siku zote muonekano mzuri ni muhimu hivyo itakuongezea motisha ya kupenda kuwa na muonekano mzuri wa kiurembo.
6. Penda kazi yako na vaa kutokana na mazingira ya kazi yako, kama utaipenda kazi yako mara kwa mara na kuwa makini na kazi zako itapelekea urembo zaidi kimavazi. Kazi ni sehemu ya ndani yako jaribu kuvaa kutokana na kazi yako kwa mfano karani, afisa maendeleo ya jamii, daktari, mwanasheria, na kazi mbalimbali basi jitahidi uvae mavazi yanayolandana na mazingira na hivyo kuongeza ufanisi na ubora katika kazi yako kwasababu tayari utajijengea ujasiri kimuonekano.
7. Epuka majungu na ishi vizuri na watu, mara nyingi majungu hupelekea ugomvi na hasira na hivyo kupelekea sura kukunjamana na kukosa amani pia. Kwa kuepuka hali ya ugomvi itajenga furaha wakati wote na sura yenye tabasamu hivyo urembo wa nje utajitokeza kirahisi zaidi. 

KUMBUKA: Kuwa mrembo ni rahisi kwa mwanamke yoyote kwakuwa furaha ya mtu huletwa na mtu mwenyewe basi jenga tabia ya kujipa furaha mara kwa mara kwa kujiaminisha kuanzia katika akili na utakuwa mwenye ngozi nzuri kama mwanamke na afya njema.

No comments:

Post a Comment